UDHALILISHAJI BADO SUALA LINALOPASUA VICHWA VYA WADAU MBALI MBALI PEMBA
Na Amina Ahmed Moh’d Pemba
WANANCHI wa maeneo ya Mwambe Pemba wamesema bado wanakabiliwa na changamoto kadhaa katika kupambana na vitendo vya udhalilishaji wa kijinsia na ajira za utotoni ni pamoja na muhali na wanajamii kutokuwa na umoja na mashirikiano.
Wakizungamza na waandishi wa Habari katika mkutano wa wadau wa kupambana na vitendo vya udhalilishaji na utumikishwaji wa watoto katika Ofisi za KUKHAWA Chake Chake, wamesema kumekuwepo baadhi ya wanajamii ambao wanashindwa kutoa mashirikiano pindi vinapotokea vitendo viovu jambo ambalo linapelekea kuongezeka kutokea kwa vitendo hivyo.
Kwa upande wake mkurugenzi wa jumuiya kupunguza umasikini na kuboresha Hali za wananchi 'KUKHAWA' Hafidh Abdi Said, amesema wameamua kushirikiana na waandishi wa Habari katika mradi wa KATAA UKATILI WA KIJINSIA DHIDI YA WANAWAKE NA WATOTO kwani waandishi wa Habari ni wadau muhimu katika kuibua na kupambana na vitendo vya udhalilishaji na utumikishwaji wa watoto.
Nae mratibu wa chama cha waandishi wa Tanzania TAMWA Kisiwani Pemba Bi. Fathiya Mussa Said, amesema utafiti walioufanya wamegundua kuwa miongoni mwa sababu zinazopelekea kukithiri kwa vitendo vua udhalilishaji ni vijana kulala magetoni na uangaliaji wa televisheni nyakati za usiku.
Mratibu wa Jumuiya ya Watu Wenye Ulemavu wa Akili Pemba Khalfan Amour Mohammed, amesema miongoni mwa maeneo ambayo yameathirika na ajira za utotoni na vitendo vya udhalilishaji ni maeneo ya Mwambe na Ndagoni.
Mradi wa KATAA UKATILI WA KIJINSIA DHIDI YA WANAWAKE NA WATOTO MKOA WA KUSINI PEMBA unatekelezwa na jumuiya ya KUKHAWA Kwa ufadhili wa taasisi ya Foundation For Civil Society.
Comments
Post a Comment