KUTANA NA VIJANA WA KIKE WALIYOAMUA KUVUNJA UBAGUZI WA KIJINSIA KATIKA SEKTA YA KILIMO
Na Masoud Juma, Unguja.
“KUTOKANA na ukosefu wa ajira, kwa hiyo baada ya kuona fursa ya kilimo na hapo tulikua tushapata mafunzo, tukaamua kujitoa majumbani na kuanza kujikita katika sekta hiyo ili tuweze kupata maendeleo” anasema Subira.
Nchini Tanzania sekta ya kilimo ndio uti wa mgongo wa uchumi wake, watu wengi hujiajiri katika sekta hiyo lakini kwa bahati mbaya si wanawake wengi wamejitokeza katika kufanya shughuli za kilimo
Marekebisho ya kiuchumi yamesaidia sana kufungua sekta ya kilimo kuanzia kwenye usindikaji, usafirishaji na uuzaji wa bidhaa za kilimo yameifanya sekta hii kukua na kuwa na maslahi makubwa kwa wananchi.
Hali imekua tofauti kwa kijana Zainab Zubeir Juma na wenzake kwani wao wameamua kuitumia fursa ya kilimo kama ndio mkombozi wao na Zainab nae amesaidia sana kushawishi wanawake wenzake ambao hawakuwahi kufikiria kujikita katika sekta hiyo kujiunga nae katika shughuli za kilimo na kujipatia kipato.
Zainab aliamua kujiingiza katika kikundi kinachojulikana kwa jina la UMASIKINI MWIKO kilichopo katika shehia ya Kizimbani ambacho kimewashajihisha vijana wengi hasa wa kike kujiingiza katika sekta hiyo na hivyo kujikomboa kiuchumi.
Zainab anategemea kukua zaidi katika sekta hiyo na mwisho afikie malengo yake ya kuwa mkulima mkubwa zaidi hapa visiwani Zanzibar.
“familia ilipokea vizuri na walinipa Baraka zao kwa ajili ya kilimo na hakukua na changamoto wala kizuizi chochote kwa mimi kujiingiza sekta hiyo” alisema Zainab.
Aidha Zainab anatoa wito kwa vijana wenziwe wa kike kuacha kuchagua shughuli za kujiingizia kipato, alimradi kazi iwe halali, Zainab anasema hakuna kazi maalum kwa ajili ya mwanamke au mwanamme.
Ushiriki wa wanawake katika sekta ya kilimo ilionekana imepwaya sana kwa upande wa wanawake, na watu hushangaa khasa kumuona mwanamke anajiingiza katika sekta hiyo.
Mwenyekiti wa kikundi cha UMASIKINI MWIKO Othman Ali Ibrahim anasema katika kikundi hicho wanauona mchango mkubwa wa wanawake katika kikundi hicho na wao kama wanakikundi wanawategemea sana wanawake katika ukuaji wa kikundi chao.
“fursa hii ya ujasiriamali ni nzuri sana na ina faida sana hivyo nawasihi vijana wa kike na wa kiume kujiunga na sekta hii kwani ina faida katika kujiendeshea maisha”.
Aidha ndugu Othaman aliongeza kwa kuwashauri vijana wa kike kuwa kilimo si kwa ajili ya wanaume ama wazee tu bali ni kwa ajili ya watu wote na kitaweza kuwasaidia kujikomboa kiuchumi na kujiletea maendeleo endelevu.
Ripoti ya Shirika la chakula na kilimo la Umoja wa Mataifa ya mwaka 2020 imeelezea kuwa elimu waliyokuwa nayo wanawake katika nchi za Afrika imewafanya kufikia asilimia 60 ya nguvu kazi inayotumika katika kilimo cha kaya wakiwajibika katika uvunaji, uhifadhi wa mavuno na ufugaji wa wanyama na pia wanawajibika katika lishe ya familia katika jukumu la kuandaa mlo wa familia.
Ndugu Rahma Nyakongo kutoka taasisi ya KILIMO HAI anasema kuwa wamekua na mradi wa GAPE ambao umekuja mahususi kuwasaidia mabinti waliopitia ukatili wa kijinsia ili waweze kusimama na kujitegemea wenyewe kiuchumi.
“kama tunavojua sasa mambo ya udhalilishaji wa kijinsia yamekua ni mengi na ya kutisha, kwa hivyo sisi tunawachukua mabinti hawa na kuwapa mafunzo ni kwa namna gani wanaweza kuendelea na maisha na kujikinga na vitendo vingine vya udhalilishaji”, alisema.
Rahma aliongeza kuwa wao wanaamini kuwa wakishawasaidia vijana hawa kupata msaada wa kisaikolojia wataweza kuwa mabinti bora na kuweza kujikita katika masuala ya kilimo na ujasiriamali.
“Taasisi ya KILIMO HAI inaendelea kuwafuatilia vijana hawa ni kwa namna gani wanaendelea na tunawapa muongozo mzuri ili wazidi kufanikiwa”.
Nae sheha wa shehia wa Kizimbani amezungumzia changamoto zinazowakumba wakulima wa eneo hilo huku akiutaja wizi na wanyama ambao huvuruga na kuharibu mazao ya wakulima.
“kina mama sasa hivi ndio wakulima wakubwa hasa hwa vijana wa kike ndio wana kipaombele kikubwa katika masuala haya ya kilimo.” Alisema sheha huyo.
Ametoa wito kwa wakulima kuendelea kufanya doria ili waweze kugundua ni kina nani wanaharibu ama kuiba mazao yao na yeye yuko tayari kutoa ushirikiano ili kuwapeleka katika vyombo vya sheria wanaofanya vitendo hivyo.
Kipindi hiki kinamalizia kwa kusikiliza maoni ya vijana wa kike waliomo katika kikundi cha UMASIKINI MWIKO na wote wanatoa ushauri kwa vijana wenzao kutochagua kazi kwani wao kazi hiyo ya kilimo inawasaidia kwa kiasi kujikwamua na umasikini.
Comments
Post a Comment