JUMLA YA VIKUNDI 42 VYA KIJALUBA VIMEPATIWA VITENDEA KAZI KWA AJILI YA KUANZA KWA UTEKELEZAJI WA MRADI
Na- ASHA AHMED
VIKUNDI 42 vya Unguja na Pemba vimekabidhiwa visanduku maalum ambavyo vimekusanya vifaa mbalimbali kwa ajili ya kuanza rasmi utekeleza wa mradi wa Kijaluba.
Akizungumza na wahusika wa vikundi hivyo, mratibu wa mradi huo kutoka TAMWA Zanzibar Nairat Ali, alisema kwa upande wa Unguja wana jumla ya vikundi 20 na kwa upande wa Pemba ni 22 ambavyo awamu hii ya majaribio itakuwa na vikundi 42.
Aidha alisema ili kuona kuwa vikundi hivyo vinaendelea kufanya kazi zao walizokusudia katika mradi huo wamekabidhi visanduku kwa ajili ya watu kuanza kuweka hakiba (hisa) ili kuweza kujiimarisha kiuchumi.
Alisema katika vitendea kazi vilivyokabidhiwa ni pamoja na kalkuleta ambazo zitawasaidia katika kupanga mahesabu yao, buku kwa ajili ya kuhifadhia taarifa zao, vibuku vidogo vidogo kwa kila mwanachama, na kufuli tatu kwa ajili ya usalama wa kisanduku, mistari, kalamu, wino wa kufutia na muhuri kwa ajili ya kuonesha idadi ya hisa alizonazo mwanachama.
Msaidizi wa mradi wa KIJALUBA ndugu Khairat Haji, alisema, Tamwa Zanzibar kupitia mradi wa kijaluba, wamejipanga kutumia vyombo vya habari katika kupaza sauti kupitia watu wenye ulemavu kuhakikisha kuwa wanatetea haki zao na kuonesha nguvu zao katika jamii katika kufikia malengo endelevu.
Alisema vitu vilivyokabidhiwa ni moyo wa vikundi kwani ili kikundi kiweze kuendelea ni lazima kuwe na vitendea kazi ambavyo wamekabidhiwa hivyo aliwahimiza wanakikundi kuvitunza na kuvitumia vifaa hivyo ili lengo lilokusudiwa liweze kufikiwa.
Khairat aliongeza kuwa lengo hasa ni kuwanyanyua watu wenye ulemavu kiuchumi na kuwafanya wajulikane katika jamii, kuwa wanaweza na wanaweza kujitegemea na kuepukana na utegemezi na dhana potofu kuwa watu wenye ulemavu ni wa kusaidiwa tu.
Alisema mipango yao hasa ni kusimamia na kuhakikisha kwamba kila kitu kinachohusiana na mradi ikiwemo sheria na kanuni zilizopo na malengo yanafikiwa kwa wakati.
"Lengo letu ni kuona malengo tunayafikia ili tuweze kuendelea na mradi huu kwani tukumbuke kuwa mradi huu ni wa majaribio kwa muda wa miaka miwili" alisema.
Ndugu Ali Machano ambae ni afisa mradi kutoka Shirikisho la Jumuiya za Watu wenye Ulemavu Zanzibar alisema katika uanzaji wa mradi pia watatoa mafunzo kwa walimu wa ndani ya shehia pamoja na wawakilishaji wa jumuiya ya watu wenye ulemavu kwa ajili ya kuwafundisha namna ya kufanya utaratibu wa kuweka na kukopa kwa mujibu wa taratibu zilizowekwa na mradi wa kijaluba na wafadhili wao wa chama cha watu wenye ulemavu cha norwe.
Bi Nairat Ali alifahamisha kuwa mafunzo hayo yatakuwa kwa ajili ya kuwafundisha walimu lengo ni kujua jinsi ya utekelezaji wa mradi kwani wao ni wasimamizi wakuu katika shehia na badae wataripoti kwa ofisa wa fildi.
Nao, wanakikundi cha TUSTAHAMILI kilichopo Mtende wilaya ya Kusini Unguja walisema wamefurahishwa na uwepo wa mradi huo na kusema kuwa mradi utawasaidia sana katika kujikwamua na umasikini.
Kikundi cha TUJIKOMBOE kilichopo katika shehia ya Ngananani wilaya ya Kusini Unguja waliahidi kuvitumia na kuvitunza vifaa walivyokabidhiwa ili lengo la mradi liweze kufikiwa.
Mradi wa Kijaluba ni mradi wa kuwasaidia watu wenye ulemavu kiuchumi ambao unatekelezwa kwa mashirikiano na TAMWA Zanzibar pamoja Shirikisho la Jumuiya za Watu wenye Ulemavu Zanzibar kwa ufadhili wa Chama cha watu wenye Ulemavu cha Norway.
Comments
Post a Comment