ALIEKOMBOA WANAWAKE KUTOKANA NA UMASIKINI NI MUANZILISHI WA KIKUNDI CHA “TUPO WENYEWE”.
Na Masoud Juma, Unguja.
NI KIPINDI kirefu kilichopita ilikua si rahisi kuona wanawake wakijishughulisha na shughuli zozote za kiuchumi hapa visiwani Zanzibar.
Hata baada ya kuanza kuingia kwenye shughuli za kiuchumi bado wanawake hawakuwa katika ajira rasmin, ambapo kwa mujibu wa kituocha taifa cha takwimu ni asilimia sitini ya wanawake wote wanajishughulisha na ajira zisizo rasmin.
Katika kuhakikisha kuwa anajikomboa kiuchumi bi Subira Khamis Ali mkaazi wa Bumbwini Misufini aliamua kujishughulisha na kazi za ususi wa mikoba, vipepeo na makawa na kuviuza sehemu mbali mbali zenye uhitaji.
Baada ya kuona kuwa anafaidika kwa kiasi na kupata ari na moyo wa upambanaji bi Subira aliamua kuanzisha kikundi cha ujasiriamali cha wanawake ambacho kinajishughulisha na masuala hayo ya ususi kinachojulikana kwa jina la TUPO WENYEWE.
Kikundi hicho chenye jumla ya wanachama 12 ambapo makazi yake yapo wilaya ya Kaskazini B kijiji cha Bumbwini Misufini wanasema pamoja na kujipatia kipato lakini shughuli zao zinasaidia sana kutunza mila za kizanzibari.
Bi Subira amewasaidia wanawake 12 kujikomboa kiuchumi kwa kujiunga na kikundi hicho ambapo kwa sasa wanatumia ujuzi wao wa kusuka mikoba na vitu mbalimbali vya ukili kwa ajili ya kujiongezea kipato.
Bi Subira anasema alianzisha kikundi hicho kwa cha ususi wa mikoba, makawa na vipepeo, ameona ili asikomboke pekeake ameona bora wakomboke wanawake wengi ambapo kwa sasa wapo 12 na yeye ndo mwenyekiti.
“Kwa sasa biashara ipo vizuri watu wanaunga mkono, angalau tunapata pesa kiasi angalau za kununulia sabuni za kuendeshea mambo yetu”. Anasema bi Subira.
Bi Subira anatoa wito kwa wanawake wa kizanzibari wasikae nyuma nyuma katika kufanya shughuli mbalimbali za maendeleo kazi ili waweze kusaidia familia zao na kujikomboa kiuchumi huku akitolea mfano kwa mama Samia ambae kwa sasa ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Nae Afisa Utamaduni wa Wilaya ya Kaskazini B Ismail Abdalla Abdillah anasema wanawasaidia wajasiriamali hawa kwa kuwapa mafunzo tofauti tofauti kwa ajili ya utengenezaji wa vitu vya sanaa ili kuendeleza vipaji na kutunza utamaduni wa mzanzibari.
Pia wanatumia fursa za matamasha na maonesho mbalimbali kuwapeleka wajasiriamali hao ili kutangaza na kuuza bidhaa zao.
Ndugu Ismail anaitaja changamoto ya soko kama ni adui mkubwa wa maendeleo ya wajasiriamali hawa kwani watu wengi wameacha kutumia vitu vya asili hivyo inapelekea kupungua kwa wateja.
Ametumia fursa hii kuwashauri wajasiriamali kuwa wabunifu zaidi ili kutengeneza bidhaa za kuwavutia wateja kwa uzuri na ubora wa bidhaa zao.
Wakizungumza na mwandishi wa Makala hii watumiaji wa bidhaa hizo wamesema ni vizuri kutumia vifaa vya asili kwani ni madhubuti na vinadumu kwa muda mrefu.
“vifaa vya asili ni vizuri khasa, kwanza ni madhubuti, vinadumu mda urefu lakini pia ni vizuri ukivitumia unaonekana mtu wa tofauti sana”. Anasema bi Fatma Rajab mkaazi wa Bumbwini.
Nae bi Halima Khamis ameongeza kuwa bidhaa zipo vizuri na zinasaidia katika kutunza mazingira na kupatikana hifadhi ya vitu kwa kutumia mkoba wa ukili wa asili.
Nae mwalim wa wajasiriamali ndugu Mhidini Ramadhan anasema kuwa kwa sasa serikali imewekeza na kutoa fursa nyingi kwa wajasiriamali kwa kuwapatia mikopo na mitaji ya kuendeshea biashara zao, hivyo amewanasihi wajasiriamali hasa wanawake kuchangamkia fursa hiyo ili kukuza biashara zao.
Kikundi cha TUPO WENYEWE kinawakaribisha wazanzibari wote kuwaunga mkono kwa kununua biashara zao na wao wapo tayari kupokea oda mbalimbali na wanaahidi watazitengeneza kwa ubora.
Comments
Post a Comment