WAANDISHI WAASWA KUSAIDIA KUTOA ELIMU KWA JAMII JUU YA MATUMIZI SAHIHI YA RISITI ZA ELEKTRONIKI NA ULIPAJI WA KODI.
NA AMINA AHMED MOH’D, PEMBA
Alisema kuwa, waandishi wa Habari ndio daraja la mawasiliano hivyo, ni vyema kuitumia taaluma yao ya uwandishi wa habari katika uwandaaji wa makala na vipindi vya kila siku kwa lengo la kuielimisha jamii.
Aliyasema hayo alipoua akizungumza na waandishi wa habari katika mkutano wa maadhimisho ya siku ya uhuru wa vyombo vya habari, huko ukumbi wa TASAF Chake chake uliyoandaliwa na klabu ya waandishi wa habari wa Pemba (PPC) kwa ufadhili Umoja wa Klabu za Waandishi wa Habari Tanzania UTPC pamoja na Mamlaka Ya Mapato Zanzibar ZRA.
"Maadhimisho haya ni muhimu na elimu mutakayoipata hapa itasaidia sana kuwajengea uwelewa juu ya masuala ya kodi, yatawasaidia kuandika habari za kweli, zenye uweledi na zilizofanyiwa utafiti wa kutosha, naomba tuyatumie mafunzo haya kwa vitendo", alisema.
Aidha alisema, serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inayoongozwa na dk. Hussein Ali Mwinyi inahimiza sana ulipaji wa kodi kwa kupitia mifumo mipya, ambapo ni jambo muhimu na inahitaji wananchi wengi kujengewa uwelewa.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa klabu ya waandishi wa habari wa Pemba (PPC) Bakar Mussa Juma alisema, PPC ni miongoni mwa klabu 28 zilizopo Tanzania chini ya mwevuli wa umoja wa vilabu vya habari (UTPC).
Alieleza, PPC katika kuadhimisha siku ya uhuru wa vyombo vya habari imeamua kuwapatia elimu ya kodi na umuhimu wa matumizi ya risiti za elektroniki waandishi wa habari ikiwa ni njia moja ya kuhakikisha mapato yanaingia katika sehemu husika.
Akiwasilisha mada Afisa kutoka mamlaka ya mapato Zanzibar ZRA Pemba Khairat Said Soud alisema, changamoto zinazotokana na biashara katika ukusanyaji wa kodi ni wafanyabiashara wengi kutokufanya usajili na kupelekea uvunjaji wa mapato.
"Vile vile wafanyabiashara kutokutoa risiti na wananchi kutokua na mwamko wa kudai risiti, kutoa taarifa za mauzo zenye viwango vya chini ni miongoni mwa changamoto ambazo mamlaka inakabiliana nazo wakati wa ukusanyaji wa kodi", alisema.
Kwa upande wao waandishi wa habari walisema, suala la ulipaji wa kodi linahitaji uzalendo hivyo, ni vyema ZRA ikaandaa utaratibu wa kutoa elimu kwa jamii ili ipate uwelewa mpana juu ya ulipaji wa kodi na kudai risiti pale wanaponunua bidhaa.
Maadhimisho ya siku ya uhuru wa vyombo vya habari duniani huadhimishwa kila ifikapo Mei 3 ya kila mwaka, ambapo kwa mwaka huu kauli mbiu ya siku hiyo ni "KUUNDA MUSTAKBALI WA HAKI, UHURU WA KUJIELEZA KAMA KICHOCHEO CHA HAKI NYENGINE ZA BINAADAMU".
MWISHO.
Comments
Post a Comment