JAMII YAASWA UJUMUISHAJI WA WATU WENYE ULEMAVU HASA WANAWAKE KATIKA NAFASI ZA UONGOZI
Na Masoud Juma, Unguja.
Jamii imetakiwa kuwajumuisha watu wenye ulemavu hasa wanawake katika masuala mbali mbali ya maendeleo hapa nchini ikiwemo katika Nyanja za kijamii, kiuchumi.
Bi Mwandawa anasemaa kuwa watu wenye ulemavu ni watu wenye uwezo mkubwa wa kiakili na fikra, hivyo mapungufu yao yasiwakoseshe haki ya kuiletea maendeleo jamii yao ama kutengwa na kuonekana kama watu wasioweza.
“ulemavu sio ugonjwa, ni mapungufu ambayo mtu huzaliwa nayo ama humkumba wakati wa makuzi yake, hivyo ni bora jamii ikaangalia utu kwanza na kumuheshimu mtu mwenye ulemavu na kumshirikisha katika shughuli mbalimbali za kimaendeleo” anasema.
Bi Mwandawa ni mtu mwenye ulemavu na ni mwanaharakati wa muda mrefu wa kutetea haki za watu wenye ulemavu hapa Zanzibar na anasema hali yake ya ulemavu haimzuii kuwa kiongozi bora wa kusimamia taasisi kubwa kama SHIJUWAZA ambayo inajumuisha takriban jumuiya 12 za watu wenye ulemavu.
“mimi ni mtu mwenye ulemavu wa mguu, na ni mwanamke lakini nna uwezo mkubwa wa kifikra wa kusaidia taasisi yangu isonge mbele, hivyo sioni sababu ya kuwaficha ama kuwatenga watu wenye ulemavu hasa hawa wa kike katika kusaidia maendeleo ya nchi yao”.
Ndugu Mohammed Ali Vuaa ni mtu mwenye ulemavu wa uoni na ni mfanyakazi katika Shirikisho la Jumuiya Watu Wenye Ulemavu Zanzibar anasema kuwa ni muhimu kuwa na jamii jumuishi kwani itasaidia kuwainua watu wenye ulemavu na kuacha kuwa tegemezi, Mohammed anatilia mkazo pia suala la kuwashirikisha zaidi watu wenye ulemavu wanawake kwani wao ndio hukumbwa zaidi na changamoto ya kufungiwa na hata kukosa haki ya msingi ya kupata elimu.
“kwa mfano tunae katibu mkuu pale wizarani bi Abeda ni mtu mwenye ulemavu, lakini anapiga kazi kweli na hiyo iwe ni mfano tosha kwa jamii hata kwa serikali yetu pia kutokuwaacha nyuma watu wenye ulemavu kwani wanao mchango mkubwa katika ujenzi wa taifa hili”
Mohammed alisisitiza kuwa ili ujumuishi upatikane ni lazima pia kuzingatia kila kitu kiwe ni kwa ajili ya watu wote akitolea mfano hata aina ya majengo yanayojengwa yawe na miundombinu ambayo kila mtu atafikia bila kupata kikwazo chochote.
Nae Mwenyekiti wa Baraza la Taifa la Watu wenye Ulemavu Zanzibar bi Salma Saadat anasema yeye anamshukuru Rais Mwinyi kwa kumpatia nafasi hiyo ya kuliongoza baraza ambalo kwa ujumla anapata nafasi ya kutatua changamoto mbali mbali za watu wenye ulemavu, hivyo ametoa rai hata kwa taasisi binafsi kuendelea kuwaamini watu wenye ulemavu hasa wanawake kwani ni watendaji wazuri.
Kwa upande wake mwenyekiti wa SHIJUWAZA bi Mwandawa ameiomba serikali kusimamia masuala ya ujumuishaji ikiwemo miundombinu, mafunzo ya lugha za alama, kutoa nafasi za uongozi ili kuionesha jamii kwamba watu wenye ulemavu si watu wa kupewa tu bali na wao wanaweza kuwa ni sehemu ya maendeleo ya taifa ikiwa watawekewa mazingira wezeshi.
Mwishoni mwa mwaka 2022 Serikali ya Mapiduzi Zanzibar ilipitisha sheria mpya ya watu wenye ulemavu ambayo kwa kiasi kikubwa imetatua changamoto mbalimbali na kuweka misingi mizuri kwa ajili ya kuwainua watu wenye ulemavu katika sekta mbalimbali.
Comments
Post a Comment