WANAWAKE WAJASIRIAMALI WATAKIWA KUTUMIA VIZURI TEKNOLOJIA ILI KUJINUFAISHA KATIKA BIASHARA ZAO.


NA  MASSOUD JUMA , UNGUJA.

Naibu Spika wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar Mheshmiwa Mgeni Hassan Juma amewataka wajasiriamali wanawake kutumia vizuri teknolojia na mitandao ya kijamii  na kuangalia ni kwa namna gani teknolojia hiyo inaweza kuwasaidia kukuza biashara zao na ustawi wa jamii kwa ujumla.

Mheshmiwa Mgeni alitoa wito huo wakati  akifungua rasmi Jukwaa la pili la wajasiriamali Zanzibar lililoandaliwa na taasisi ya The Warrior Women Foundation lililofanyika siku ya Jumamosi ya tarehe 11 mwezi wa 3 mwaka 2023  huko katika ukumbi wa Bolilo Bwawani Mjini Unguja.

Katika shughuli hiyo Mheshmiwa Mgeni aliwaasa wajasirimali kujiamini na kusimama imara katika kutekeleza majukumu yao na shughuli mbalimbali za ujasiriamali.


Katika jukwaa hilo Mheshmiwa Mgeni alisema kuwa kuna changamoto kubwa ya masoko kwa wajasiriamali wa zanzibar ambalo linasababishwa na vitu mbali ikiwemo namna ya kuhifadhi bidhaa,utafutaji wa rasilimali na nyenginezo , hivyo aliwataka wakufunzi  waliohudhuria katika jukwaa hilo wawasaidie wajasiriamali hao wadogo ni kwa namna gani wanaweza kupata masoko ambayo ni endelevu.

Aidha Mheshmiwa Mgeni aliwataka wajasiriamali kuwa wabunifu na  kutumia fursa ya utamaduni wetu wa mzanzbari kutengeneza bidhaa mbalimbali zitakazovutia soko la nje ya nchi na hivyo itasaidia pia kutangaza utamaduni wetu.

Nae Mrajis wa asasi za kiraia ndugu Ahmed Khalid amesema serikali inathamini sana juhudi za wajasiriamali nchini  na ndio maana serikali ya awamu ya nane inafanya  jitihada ya kutaka kuwatambua rasmi wajasiriamali wote  wa zanzibar.

Mrajis aliongeza kuwa ni muhimu kwa wajasiriamali kutumia fursa ya jukwaa hilo kujifunza masuala ya ujasiriamali ili kuweza kuboresha shughuli zao.

Akielezea lengo la kuanzishwa kwa jukwaa hilo Mkurugenzi Muanzilishi wa taasisi ya The Warrior Women Foundation bi Sabra Issa Machano alisema kuwa lengo la kuanzishwa kwa jukwaa hilo ni kuwasaidia wajasiriamali wadogo na kuwaonesha fursa mbalimbali pamoja na kupewa mafunzo kuhusu fedha na namna ya kukuza biashara zao.

Bi Sabra aliongeza kuwa changamoto kubwa inayowakumba wajasiriamali ni afya  zao hasa ya akili na msongo wa mawazo lakini pia kukosa elimu ya namna mbalimbali za kupita ili kuendeleza biashara zao.


Bi Lailat Dude ni mjasiriamali mdogo, nae alisema anaishukuru sana taasisi ya The Warrior Women Foundation kwani ameongeza fikra na uelewa na namna sahihi ya kutumia mtandao ili kujinufaisha kiuchumi na anaamini hiyo itakua ni njia sahihi ya kumkuza katika biashara zake. 

Bi Hafsa Said ambae ni mjasiriamali nae alisema amefaidika sana na elimu aliyoipata hapo kwani amepata kujifunza mambo mbali mbali ya namna ya utunzaji fedha lakini pia kufahamu umuhimu wa afya yake kama mwanamke .

Bila ya shaka majukwaa kama haya ni muhimu sana katika kukuza uelewa wa wanawake katika masuala mbali mbali hasa ya kiuchumi lakini pia yanawasaidia kukutana na wadau na kuongeza fursa katika kujifunza zaidi kwenye mambo yanayohusu maisha yao.


Comments

Popular posts from this blog

BARABARA 19 KUJENGWA KWA KIWANGO CHA LAMI PEMBA KUKAMILIKA DISEMBA 2024.

WAZAZI ZIDISHENI KUFUATILIA NYENENDO ZA WATOTO HUSUSAN NI VIJANA .

UONGOZI WA WILAYA CHAKE CHAKE KFHI WAPONGEZA JUHUDI