Serikali kusaidia Wanawake wajasiriamali



 Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imeahidi kusaidia vikundi vya  kina mama ili viweze kupata mikopo na kujikwamua kimaisha.

 

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla ametoa kauli hiyo alipofanya mazungumzo na Uongozi wa Umoja wa wanawake Tanzania (UWT) waliofika kujitambulisha Ofisini kwake Vuga Jijini Zanzibar.

 

Mhe. Hemed ambaye pia ni Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya CCM Taifa amesema Serikali inatoa Mikopo ya gharama nafuu kwa vikundi vya wajasiriamali kwa lengo la kuwawezesha kujikwamua kiuchumi na kuwaahidi kina mama kuwa Serikali inatoa kipaumbele kwa wanawake ili waondokane na utegemezi.

 

Mhe. Hemed ameeleza kuwa dhamira ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi ya kutenga fedha kwa ajili ya mikopo kwa vikundi vya wajasiriamali  ni  kuwawezesha wananchi kujikwamua kiuchumi.

 

Sambamba na hayo Mhe. Hemed ameupongeza Uongozi wa UWT kwa kuandaa mpango kazi ambao umelenga kuiletea mabadiliko Jumuiya hiyo hasa mpango wa kuanzisha vitega uchumi kwa kila Mkoa hatua ambayo itasaidia Jumuiya hiyo kuacha utegemezi katika kuendesha shughuli za kila siku.

 

Amesema,  Chama Cha Mapinduzi kimeelekeza kuboresha vitega uchumi na kubuni vyanzo vipya vya mapato kwa Jumuiya zake ili kurahisisha  uendeshaji wa shughuli za Chama za kila siku.

 

Pamoja na hayo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar amewapongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi kwa kuendelea kuwaletea maendeleo watanzania ndani ya kipindi kifupi cha uongozi wao.

 

Aidha Mhe. Hemed amewasihi viongozi hao kuwa wavumilivu na kutovunjika moyo kwa changamoto mbali mbali zitakazojitokeza katika kutekeleza majukumu yao ya kila siku.

 

Kwa upande wake Makamu Mwenyekiti wa Umoja wa wanawake Tanzania  Bi. Zainab Shomari amemueleza Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kuwa UWT imejipanga kufanya mabadiliko kwa kujiimarisha kimaendeleo kiutendaji, kisiasa na kiuchumi.

 

Aidha ameeleza kuwa Umoja wa Wanawake Tanzania umefurahishwa kwa juhudi za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kujenga Hospital zenye huduma za Mama na Mtoto hatua ambayo itasaidia kumaliza changamoto ya usumbufu wa kina mama wanapofata huduma hizo na kupunguza vifo vya mama na mtoto.


Comments

Popular posts from this blog

BARABARA 19 KUJENGWA KWA KIWANGO CHA LAMI PEMBA KUKAMILIKA DISEMBA 2024.

WAZAZI ZIDISHENI KUFUATILIA NYENENDO ZA WATOTO HUSUSAN NI VIJANA .

UONGOZI WA WILAYA CHAKE CHAKE KFHI WAPONGEZA JUHUDI