MWANAMKE WA MFANO ALIESHIKA NAFASI YA UWAKILISHI AWAMU 2, KUPITIA KURA ZA WANANCHI ALIELETA MAENDELEO



NA ASIA MWALIM - UNGUJA 

WAKATI Tanzania na Zanzibar zinatanua wigo wa demokrasia na utawala bora, juhudi za kupunguza pengo kati ya wanawake na wanaume zinaendelea na kupata mafanikio kiasi.

Hilo limedhirika kutokana na nchi hizo kusaini mikataba ya kikanda na Kimataifa kwamba itazingatia usawa wa kijinsia kati ya wanawake na wanaume katika uongozi.

Wakati huu wanawake wa Zanzibar wanathubutu kugombea na kushinda katika nafasi mbaali mbali za uongozi, ingawa nafasi za kuteuliwa zinaonekana  zimekua ni nyingi zaidi.

Mwanaasha Khamis Juma, Mwakilishi wa Jimbo la Dimani ni miongoni mwa mwanamke wa kupigiwa mfano, kwa kushika nafasi hiyo kwa khatamu 2, kupitia uchaguzi mkuu unaofanyika kila baada ya miaka 5.

Mwanamke huyo amekua mfano kwa wanawake wengine Zanzibar kutokana na harakati anazopitia katika kuhakikisha anaendelea kuwa kiongozi bila ya kubabaishwa na wale wasiopenda maendeleo ya wanawake.

Alisema jitihada zake katika uongozi mara zote huwa hazimuachi nyuma, kwani anajituma, na kujitoa kwa ajili ya wananchi na kufanya kazi kuliko hata wanaume.

Hatua ya kuongoza nafasi ya uwakilishi sio jambo dogo, lakini unapokuwa tayari na kujikubalisha kwa jamii unayoiongoza, hawahitaji jinsia bali ni namna gani unawaongoza na kuwatumikia.

Akizungumzia kuhusu ushiriki wa wanawake kwenye uongozi, mwakilishi huyo, alisema kwa sasa hali sio mbaya kwani wanawake wanagombea nafasi mbali mbali za uongozi na wanashinda vizuri.

Aidha alisema safu ya uongozi kwa wanawake kupitia Chama Cha Mapinduzi CCM na upande wa serikali ipo vizuri, ingawa idadi kubwa ya nafasi wanazopata wanawake ni katika uteuzi kwenye nafasi mbali mbali.

Mwanamke huyo alisema cha kujivunia ni kwamba nafasi za wanawake kwenye baraza la wawakilishi zimeongezeka kwenye majimbo kutoka wanawake saba hadi nane, kwa mwaka 2015 hadi 2020. 

Akitolea mfano wa nafasi hizo, alisema mwaka 2020, wanaume waliojitokeza kugombea nafasi ya uwakilishi 190 na walioshinda 42, ambapo wanawake walijitokeza kugombea nafasi hiyo hiyo 61 na waliobahatika kushinda ni wanane.

Mwanamke huyo, alisema kuelekea uchaguzi mkuu wa 2025, wanawake wanapaswa kujiandaa vizuri kushiriki nafasi mbalimbali, kutokata tamaa na wajiamini kwani kwa kufanya hivyo ndiko kutakakowawezesha kuzifikia ndoto zao.

Kiongozi yoyote anapo fanya vizuri, kwa wale waliomchagua ana matumaini makubwa ya kurudi tena kwenye nafasi hiyo na mara nyengine hupewa zaidi ya hiyo.

“Dk. Mwinyi kwa kutambua umuhimu wa wanawake na kuwaaamini kwenye uongozi, amewapa nafasi mbali mbali ikiwemo nafasi muhimu kwenye ngazi za maamuzi, hii ni jambo muhimu sana”, alisema Mwanaasha.

Alimpongeza Dk. Mwinyi kwa kuwaona na kuwaamini wanawake katika kuwapa nafasi za juu, jambo ambalo linawapa moyo wanawake wengine ambao wana ndoto za kuwa viongozi. 

Sambamba na hayo aliwashauri wanawake kuendelea kujitoa zaidi katika nafasi mbali mbali, ili kufikia usawa wenye hadhi sawa katika nafasi za kugombea uongozi kati ya wanawake na wanaume.


WANANCHI WALIOMCHAGUA.

Baadhi ya wananchi wa jimbo la Dimani walisema, kutokana na uaminifu na huruma za kiongozi huyo, hawana haja ya kumbadilisha.

"Bado tumejenga matumaini kwa mwanamke huyu, ambae analiwakilisha vizuri jimbo letu, tunatamani kupata viongozi wengine wanawake kwenye nafasi nyengine" walisema.

KATIBA YA ZANZIBAR
Kwa mfano katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984, katika kifungu 21(2) kila mzanzibari anayo haki na uhuru wa kushiriki kwa ukamilifu katika kufikia uamuzi juu ya mambo yanayomuhusu na yanayohusu taifa lake.

Aidha katiba hiyo katika marekebisho ya 2010 imeeleza wazi kuwa katika kifungu nambari 67 (1) kuwa kutakuwa na wajumbe wa baraza la wawakilishi wanawake kwa idadi ya asilimia 40 wa wajumbe wote wa kuchaguliwa katika majimbo.


DIRA YA ZANZIBAR 2050
Aidha Dira ya Zanzibar katika maazimio ya 2.5.1 hadi 2.5.9 yameeleza masuala mbali mbali ya usawa wa jinsia na kuondoa unyanyasaji wa kijinsia pamoja na kuimarisha mifumo ya uwezeshaji wanawake ikiwemo kuinua na kutoa nafasi za uongozi kwa wanawake katika jamii.

Pia kuongeza fursa na kuwawezesha katika vyombo vya kutolea maamuzi na kwenye shughuli za uchumi, kijamii, siasa katika ngazi zote za utawala na huduma za sheria.

SERA YA JINSIA YA ZANZIBAR
Aidha katika sera hiyo ya jinsia sura ya 4 katika nambari 4.1 inaeleza ushiriki wa wanawake katika vyombo vya utoaji wa maamuzi katika ngazi zote ni mdogo, Hivyo serikali kwa kushirikiana na wadau wengine watachukua juhudi za makusudi kuona kuwa makundi yote na yaliyopembezoni wanapata fursa hiyo.

ITIFAKI YA SADC
SADC ambayo ni Jumuiya ya maendeleo ya nchi za Kusini mwa Afrika, ambapo mkataba wake wa kikanda uliotiwa saini mwaka 2008 unaeleza kuondoa utafauti na kuwatenga wanawake katika Nyanja mbalimbali za maendeleo na kuwasaidia katika usawa wa kijinsia nchi wanachama.

Comments

Popular posts from this blog

BARABARA 19 KUJENGWA KWA KIWANGO CHA LAMI PEMBA KUKAMILIKA DISEMBA 2024.

WAZAZI ZIDISHENI KUFUATILIA NYENENDO ZA WATOTO HUSUSAN NI VIJANA .

UONGOZI WA WILAYA CHAKE CHAKE KFHI WAPONGEZA JUHUDI