KITUO CHA HUDUMA RAFIKI CHAZINDULIWA BUMBWISUDI.
NA KHAIRAT HAJI, UNGUJA.
UMOJA wa Mataifa wa idadi ya watu UNFPA na shirika la Mfuko wa kimataifa wa watoto UNICEF wamezindua rasmi kiliniki ya huduma rafiki kwa vijana huko Bumbwisudi wilaya ya Magharibi “A” Unguja.
Kliniki hiyo imezinduliwa rasmi na waziri wa afya Zanzibar Mheshmiwa Nassor Ahmed Mazrui tarehe 15/02/2023 ambapo imekarabatiwa chini ya mradi wa Wezesha Wasichana ambao unafadhiliwa na serikali ya Canada.
Katika uzinduzi huo, UNFPA iliikabidhi wizara ya afya mashine mbili za ultra sound zitakazowasaidia kina mama wajawazito ili kubaini matataizo na kusaidia kupatikana kwa mimba salama.
Akizungumza wakati wa uzinduzi huo Mheshmiwa Mazrui alisema kuwa kliniki hiyo ya kituo cha huduma rafiki kwa vijana itawawezesha vijana kupata taarifa kwa wakati na huduma za kitaalam ili kupunguza madhara ya kiafya yanayosababishwa na kutumia njia za uzazi wa mpango bila ya kufuata ushauri maalum wa wataalam wa afya.
Aidha, mwakilishi mkaazi wa UNFPA , Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ndugu Mark Bryan Schreiner amesema idadi ya vijana wenye nguvu nchini imeongezeka, hivyo vijana wanahitaji kupata huduma na taarifa ili kuwasaidia kufanya maamuzi sahihi ikiwa ni pamoja na kuhusu afya ya uzazi.
Wezesha Wasichana ni mradi wa miaka mitano unaolenga kuboresha afya ya jinsia na uzazi, haki na ustawi miongoni mwa wasichana walio katika mazingira magumu katika wilaya 22 za mikoa ya Songwe, Mbeya na Zanzibar ambapo mpaka sasa kliniki tano za huduma za vijana zimeshakarabatiwa.
Mwisho
Comments
Post a Comment