DK MZURI ATILIA MKAZO SERA YA JINSIA KATIKA VYOMBO VYA HABARI, KUMALIZA UDHALILISHAJI MAOFISINI LAZIMA ITUMIKE IPASAVYO
NA KHAIRAT HAJI, UNGUJA
MKURUGENZI wa Chama Cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania Tamwa Zanzibar, Dk Mzuri Issa Ali Amesema sera ya jinsia kazini ndio chachu ya kupunguza masuala ya udhalilishaji maofisini.
Dk Mzuri ameyasema wakati wa uwasilishaji ripoti za madawati ya jinsia yaliyomo ndani ya vyombo vya habari ambavyo vilipatiwa mafunzo na Tamwa Zanzibar, yaliofanyika huko ofisini kwao Tunguu, Unguja.
.
Dk Mzuri ameongeza kuwa sera na madawati ya jinsia yanatakiwa kuwa ndio macho na masikio ya kuhakikisha kuwa masuala ya kijinsia yanaripotiwa vizuri maofisini.
Aidha Dk Mzuri amesema kuwepo kwa sera ya jinsia na madawati yake katika vyombo vya habari kutasaidia sana kuhakikisha kuwa habari za jinsia zinaripotiwa ipasavyo .
Ndugu Husna Mohammed ambae ni mkuu wa dawati la jinsia katika gazeti la Zanzibar leo amesema anaishukuru sana Tamwa Zanzibar kwa kuwapatia mafunzo ya kuanzisha sera ya jinsia kwani mafunzo hayo yamekuwa ni chachu pia ya kuanzishwa kwa Gazeti maalum la wanawake ambalo hutolewa kila mwisho wa mwezi. .
Said Omar kutoka Radio Jamii Mkoani Pemba, Amesema kuwa yeye kama Mhariri Mkuu wa Radio hiyo atajitahidi kuhakikisha kuwa sera hiyo inatekelezwa ipasavyo.
Aidha Ndugu Maryam Ame afisa mradi wa kuongeza nafasi za wanawake katika uongozi kutoka Tamwa Zanzibar amewataka wakuu na wajumbe wa madawati hayo kuzungumza na viongozi wao na kuona ni kwa namna gani madawati hayo yanakuwa na mamlaka katika utekelezaji wake kwa watendaji wa vyombo vya habari.
Afisa Mdhamini wa Baraza la Habari Tanzania Shifaa Hassan ametoa wito kwa wahariri na watendaji wa vyombo vya Habari kuimarisha Sera ya jinsia na kamwe isibaki katika mafaili bali ifanyiwe kazi kwa vitendo.
Sera ya jinsia katika vyombo vya habari ni muongozo wa mwenendo wa utendaji kwa wamiliki wa vyombo vya habari pamoja na wafanyakazi wote ambayo itatengeneza mazingira mazuri salama na bora kwa ajili ya kufanya kazi ndani ya vyombo vya habari.
Mafunzo ya kuanzisha Sera ya Jinsia katika vyombo vya habari kwa viongozi na waandishi wa habari yametolewa na Tamwa Zanzibar mwezi Agosti mwaka 2022 kwajili ya kupunguza masuala ya udhalilishaji na kuongeza hadhi kwa watendaji wa kike, na mpaka sasa takriban vyombo vya habari 6 Zanzibar vimeshawasilisha Sera hiyo Kwa Tamwa Zanzibar.
Comments
Post a Comment