WAANDISHI ANDIKENI MAZURI YANAYOFANYWA NA WANAWAKE KATIKA JAMII NA TAIFA YAPO MENGI YA MFANO.
NA AMINA AHMED MOH’D- PEMBA.
WAANDISHI wa habari Zanzibar wameaswa kuwaibua na kuwandika Vizuri wanawake wanaoendelea kufanya mambo Mazuri ya kuleta Maendeleo katika jamii na Taifa katika nyanja mbali mbali ili kutoa wigo kwa wanawake wengine na kusaidia kuongeza idadi ya viongozi wanawake ambao wataaminika katika Jamii.
Ametoa ushauri huo Mkurugenzi wa Chama Cha Waandishi wa Habari wanawake Tanzania Tamwa Zanzibar Dkt, Mzuri Issa Ali alipokua akizungumza waandishi wa habari vijana wa vyombo mbali mbali kutoka Unguja na Pemba ambao wanaendelea kupatiwa Mafunzo maalumu ya kujengewa uwezo juu ya kuripoti habari za wanawake kushika nafasi za uongozi katika nyanja mbali mbali sambamba na kuchochea uwajibikaji kwa maslahi ya jamii.
Alisema kwa muda mrefu wanawake wengi wamekua wakishindwa kufikia malengo ya kushika nafasi za uongozi katika ngazi mbalimbali kutokana na kuandikwa vibaya na baadhi ya waandishi na kupelekea kujengeka dhana Potofu ya kwanaume Pekee ndio wanapaswa kuwa viongozi jambo ambalo ni kinyume na Mikataba yote ya kikanda na kimataifa.
‘’Nyinyi waandishi wa habari vijana muna nafasi kubwa kuibadili hali hii, sauti zenu ni kubwa zaidi ambazo mkizitumia vizuri tunaweza kufika tunapopataka yapo mazuri tele yaliofanywa na yanayoendelea kufanywa na wanawake ambayo ni mifano ya kuigwa ’ ’alisema.
Akitoa uzoefu wa kusaidia jamii kupitia kazi ya uandishi wa habari Fatma Alloo ambae ni moja kati ya waanzishi wa chama cha Waandishi wa Habari wanawake Tanzania kuwa na Mashirikiano na watu mbali mbali ili kujenga uhusiano mwema katika utendajibkazi za kihabari.
Aidha Aliwataka wanahabari hao kujiwekea malengo pamoja na kuwa watu wenye misimamo pale wanapoamua kutafuta jambo kwa maslahi ya wanawake na umma kwa ujumla.
Akitoa ushuhuda Mwenyekiti wa Jumuia ya kupambana na changamoto zinazowakabili wajane Zanzibar (ZAWIO) Tabia Makame alisema wanawake wanaotaka kuwa viongozi wana wajibu wa kujitambua na sio kuwa warahisi kwa kila jambo.
Alisema kuna idadi kubwa ya wanawake wanaoshindwa kufikia malengo yao kwa sababu wanashindwa kujielewa na kwa hali hiyo wanajikuta wanaingia kwenye mgongano na wasiopenda kuona wanawake wakipiga hatua zaidi za kimaendeleo.
‘’ Lazima tukubali ukweli udhalilishaji kwenye sehemu za kazi upo lakini ni wachache wanaoweza kukubali kuacha kazi kwa kulinda heshima yao hivyo ni lazima nyinyi vijana wadogo mjitambue’’aliongezea.
Akitoa ushuhuda mwengine Makamu wa Rais mstaafu kutoka Chuo cha Kikuu cha Zanzibar (ZU) na Waziri wa fedha Bunge la vijana Tanzania Zainab Salum Saleh alisema wanawake wanaweza kufikia malengo yao iwapo watajitoa katika kila jambo.
Pamoja na changamoto ambazo wanawake wanapitia wanapoonesha dhamira yao ya kuwa viongozi lakini kwa pamoja hawapaswi kukata tamaa na changamoto hizo badala yake wazione kama fursa za kusonga mbele.
Sambamba na hayo aliwataka vijana wenzake wanaotaka kuwa viongozi kukimbia kabisa viashiria vya rushwa pindi wanapoviona kwa sababu kuchukua sehemu hiyo ni kujiharibu pia kuikandamiza jamii yako na kufanya jambo hilo liendelee.
Jumla ya waandishi wa habari vijana 18 kutoka Unguja na Pemba wanaendelea kujengewa uwezo kupitia mradi unaotekelezwa na TAMWA-ZNZ kwa kushirikiana na shirika la “National Endowment for Democracy – NED”.
Mwisho
Comments
Post a Comment