Mama Mariam Atoa neno kwa Wakulima wa Mwani Pemba

FATMA SULEIMAN -PEMBA.

Mke wa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi ambae ni Muasisi na Mwenyekiti wa Taasisi ya Zanzibar Maisha bora Foundation Mama Mariam  Mwinyi amewataka Wakulima wa zao la Mwani kuwashawishi vijana kujikita katika ukulima wa zao hilo ili kuweza kujikwamua na Umaskini .

Alisema zaidi ya asilimia 90 ya wakulima wa mwani ni wanawake hivyo ,waitumie mbinu ya Umama ili kuwashawishi na kuwahamasisha Vijana kuweza kulima zao hilo ,kwani ni kilimo  chenye matokeo mazuri .

Mama Mariyam aliyaeleza hayo huko Kisiwani Pemba wakati alipokua akikabidhi vifaa vya ukulima wa zao hilo kwa vikundi mbalimbali vya mkoa wa Kusini Pemba  ikiwa ni ziara maalum   ya kugawa vifaa  kwa wakulima wa Mwani, Pamoja na Watu wenye Mahitaji Maalum. 

Mwenyekiti huyo wa taasisi ya Zanzibar maisha bora  aliwataka Wakulima hao kuvitunza vifaa walivyopewa ili kufikia malengo yaliyokusudiwa.

"Nawaomba Wakulima ambao leo mumepata vifaa hivi muendelee kuvitunza ili viwe endelevu na kuwafaidisha kwa muda mrefu", alisema.

Aliwasihi kuwa na ari kubwa ya kufanya kazi ya ukulima huo kwani kufanya hivyo wataweza kupata wavumo mazuri huku ikimpa nguvu na moyo yeye kama Mwenyekiti kuona sasa wakulima wamepatiwa Ari ya kufanya kazi.

"Mukizidisha bidii na moyo wa kujituma zaidi katika kilimo hicho hata mimi nitapata hamasa kubwa zaidi ya kuwasaidia ", alieleza.

Mapema Waziri wa uvuvi na uchumi wa buluu Mh Suleiman Masoud  Makame alimpongeza Mwenyekiti huyo kwa kuzisikiliza changamoto za wakulima hao na kuzitekeleza kwa vitendo.

Awali Mkuu wa Mkoa wa kusini Pemba Mattar Zahor Masoud alisema anafarajika sana kuona Mama Mariyam Mwinyi ana mapenzi makubwa na Wazanzibar huku akiahidi atafutilia vikundi vyote waliyopewa vifaa ili kuona ni namna  gani wanavifanyia kazi na kuleta matunda mazuri.

Kwa upande wao wakulima hao walimpongeza Mwenyekiti huyo wa taasisi ya Maisha bora Foundation kwa msaada huo aliowapatia  na waliahidi kuvitunza na kuvitumia kama ilivyo kusudiwa.

Vifaa vilivogaiwa kwa Wanavikundi hao boti kubwa 1 na vihori viwili ,vifaa vya uokozi (life jacket) ,Kamba ,mashine mbili za kusagia mwani ,mashine mbili za kuchanganyia utengezaji wa sabuni pamoja na Viatu kwa wakulima wa mwani .
                   MWISHO.

Comments

Popular posts from this blog

BARABARA 19 KUJENGWA KWA KIWANGO CHA LAMI PEMBA KUKAMILIKA DISEMBA 2024.

WAZAZI ZIDISHENI KUFUATILIA NYENENDO ZA WATOTO HUSUSAN NI VIJANA .

UONGOZI WA WILAYA CHAKE CHAKE KFHI WAPONGEZA JUHUDI