Wana CCM wampokea kwa vishindo Dk Mwinyi
NA HANIFA SALIM, PEMBA
MAKAMU Mwenyekiti wa (CCM) Zanzibar ambae pia ni Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi, amewahakikishia wananchi wa kisiwa cha Pemba, kwamba katika miaka mitatu ijayo ataweka juhudi maalumu za ziada kuhakikisha ahadi zote alizoziweka zinatekelezwa.
Dk. Mwinyi alisema, atahakikisha atakaporudi kwa wananchi katika kipindi cha kampeni ahadi alizoziweka amezitekeleza, huku akiahidi kutumia nguvu zake zote katika kuwatumikia wananchi wa Visiwa vya Zanzibar.
Aliyasema hayo katika mkutano wa ndani wa mapokezi ya Makamu mwenyekiti wa (CCM) Zanzibar, Kisiwani Pemba uliofanyika katika kiwanja cha kufurahishia watoto Tibirinzi Chake chake.
Alieleza, kwa mujibu wa Ilani ya Chama cha Mapinduzi (CCM) anatakiwa atekeleze ahadi alizizoweka kwani ndio mkataba wake na wananchi, itakapofika 2025 wananchi watakua wanahitaji majibu ya ahadi alizowapa.
Alisema, nchi haiwezi kupata maendeleo bila ya uwepo wa amani, utulivu, umoja, mshikamano na maridhiriano hivyo aliwataka wananchi kuhakikisha wanalinda amani iliyopo Zanzibar.
“Nataka niseme mambo ambayo tumeyakusudia kuyafanya Pemba, tunataka kuwa ni eneo maalumu la uwekezaji la kimkakati, ili wawekezaji waje hapa na sina shaka kwani nimeshaona dalili za watu wengi kuja Pemba”, alisema.
Alifahamisha, anaposema kufunguka kwa Pemba maana yake ni kujengwa kwa Uwanja wa ndege wa Kimataifa ambao tayari fedha zimeshapatikana, kujengwa bandari ya mkoani ambayo inaendelea na ujenzi, barandi ya Shumba na Wete ambayo mipango yake ipo katika hatua nzuri.
“Barabara ya Chake hadi Wete tayari Mkandarasi yupo kazini na barabara ya Chake hadi Mkoani fedha zimeshapatikana sina shaka tukishafungua maeneo haya matatu uchumi wa Pemba utakua mkubwa zaidi”, alisema.
Alisema, baada ya kufungua kiwanja cha ndege cha kimataifa Pemba, kukamilika ujenzi wa bandari na barabara uchumi wa Kisiwa hicho utakua mkubwa zaidi na yaliyokusudiwa yataweza kupatikana.
Aidha Dk. Mwinyi alisema, kazi ya uchaguzi katika chama cha Mapinduzi (CCM) imekamilika kilichobakia sasa ni kuhakikisha viongozi wote wanashirikiana katika kukijenga chama chao vizuri zaidi.
“Umoja wetu ndio ambao utakijenga chama chetu, chama ambacho kina mfarakano, makundi hakiwezi kuwa madhubuti, tumemaliza uchaguzi walioshinda wameshinda na walioshindwa wameshindwa wasubiri nafasi nyengine itakayokuja baadae”, alisema.
Hata hivyo Dk. Mwinyi pia aliahidi, kusimamia uchumi wa chama cha Mapinduzi (CCM) ili kiweze kuyatimiza malengo yake yaliyokusudiwa.
Naibu Katibu Mkuu wa (CCM) Zanzibar Abdalla Juma Sadala (Mabodi) alisema, Chama cha Mapinduzi kimemchagua dk. Mwinyi kutokana na uungwana wake wa kutekeleza ahadi zake anapoziweka.
“DK. Mwinyi aliwaahidi wanyonge, waendesha bodaboda na leo wamefaidika, wavivu na wakulima wa mwani wote amewasaidia kwa kuwapatia vihori ambavyo vitaendesha kufanya shughuli zao”, alisema.
Akitoa salamu za Serikali Mjumbe wa kamati kuu ya Chama cha Mapinduzi (CCM) Taifa ambae pia ni Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Hemed Suleiman Abdulla alisema, dk, Mwinyi wananchi wa Kisiwa cha Pemba wanamuunga mkono kwa asilimia 100%.
“Niwaombe wananchi muliopo Pemba tuna kila sababu ya kuendelea ya kumpa mashirikiano Makamu Mwenyekiti wetu wa (CCM) Zanzibar dk. Hussein Ali Mwinyi ili umsaidie kutekeleza zaidi majukumu yake”, alisema.
Aidha alisema, Dk. Mwinyi katika Kisiwa cha Pemba amepeleka nguvu kubwa kwenye kipindi cha miaka miwili iliyopita bila kujali ubaguzi, kwa kujenga madarasa 438 na gorofa 4 za skuli za sekondari, kujenga matangi matano ya maji, miondombinu ya barabara, ujenzi wa bandari unaoendelea pamoja na ujenzi wa uwanja wa ndege wa kimataifa.
Katibu wa NEC Itikadi na Uenezi (CCM) Taifa Shaka Hamdu Shaka alisema, nyenzo kubwa iliyoifikisha nchi hii hadi kufikia hapo ni kuwepo kwa amani, umoja na mshikamano uliotawaliwa na maridhiano na mapatano ya kisiasa.
MWISHO.
Comments
Post a Comment