MKURUGENZI ZRB PEMBA JAMAL HASSAN JAMAL ATOA ELIMU KWA WAFANYA BIASHARA WETE
Na AMINA AHMED MOH’D PEMBA.
MKURUGENZI wa Bodi ya Mapato Zanzibar (ZRB) Pemba, Jamal Hassan Jamal amewataka wafanya biashara waendelee kuiunga mkono serikali yao ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa kulipa kodi kwa mujibu wa utaratibu na sheria zinavoelekeza.
Aliyasema hayo mara baada ya kuwatembelea wafanya biashara wa Mji wa Wee , ambapo ni utaratibu wao kila ifikapo Disemba ya kila mwaka kupita kwa wafanya biashara kutoa shukurani na kusikiliza changamoto, ushauri na maoni yao juu ya utendaji kazi wa ZRB.
Amesema, wafanya biashara wa Mji wa Wete kwa asilimia kubwa wamefurahishwa na ujio wa watendaji wa ZRB ambapo wamefahamu kwamba bodi inafanya kitu kizuri cha kurejesha shukurani kwa wafanya biashara.
"Kiukweli tumefikia sehemu nzuri ZRB na wafanya biashara, tumechukua changamoto zao zinazotokana na sheria zetu za kodi, viwango vya tozo ambazo wanalipa, nyengine zinatokana na uwelewa mdogo ambapo tumechukua nafasi ya kuwapa elimu",alisema.
Aidha alisema, mbali ya kupita kwa wafanya biashara kutoa elimu ya kodi pamoja na kusikiliza shida zao, ZRB imejipanga kupita katika hospitali ya Abdalla Mzee Mkoani kutoa misaada, kutoa msaada wa chakula kwa watu wasiojiweza na kufanya mabonanza yatakayohamasisha jamii.
Hata hivyo aliwataka, wananchi kufahamu kwamba wafanya biashara ni wakala ambao wamechaguliwa tu na ZRB kukusanya kodi na kuiwasilisha katika taasisi husika, na kuelewa kuwa wanaolipa kodi ni wananchi na sio wafanya biashara hivyo lazima wanaponunua bidhaa wadai risiti ya kielektroniki.
Mmoja miongoni mwa wafanya Biashara Katika Mji wa Wete Sleiman Muhammed Anad ameitqka ZRB, kuhakikisha kila mfanya biashara anatumia mashine ya kutoa risiti za kielektroniki anapouza bidhaa ili kuona kodi inaingia katika taasisi husika kama malengo yalivopangwa.
"Ni vizuri ikiwa ZRB itamuweka mfanya biashara kila mmoja katika sehemu yake katika utaratibu wa kulipa kodi bila ya kufanya ubaguzi hapo tutakwenda sawa na hatutoacha kushirikiana na ZRB", alisema.
Nae Mfanya biashara Salim Awadh Omar alisisitiza, ZRB kusimamia suala la kulipa vati kwa usawa kwa wafanya biashara wote ili kuepusha kuuza bidhaa kwa bei zisizo elekezi.
Nae Sleiman Hemed Hamad Ambae ni mfanya biashara Katika mji huo Wameitaka kuwapunguzia tozo wanazolipia kwani alisema, wafanya biashara wengine tozo ni kubwa ikilinganishwa na mauzo wanayouza kwa mwezi.
Mfanya biashara Moza Omar Said Sheha aliwataka Watendaji hao kuweka utaratibu maalum wa kuwakumbusha ulipaji deni wa wafanya biashara ili kuepeusha kulupa faini wanapochelewa ambapo alisema baadhi ya wafanya biashara wanaghaflika na kusahau.
MWISHO.
Comments
Post a Comment