MIKAKATI ILIYOUNDWA KUPAMBANA NA UDHALILISHAJI KASKAZINI PEMBA YAZAA MATUNADA WANANCHI WAPATA UELEWA KUYARIPOTI YANAPOJITOKEZA.
- Get link
- X
- Other Apps
NA - AMINA AHMED MOH’D - PEMBA.
MASHIRIKIANO yanayotolewa katika kusimamia mikakati maalum ilionazishwa na Serikali ya Mkoa wa kaskazini Pemba juu ya kupambana na vitendo vya uhalifu kwa miaka Miwili sasa imesaidia kuongeza uelewa kwa wanajamii juu ya kuripoti matukio ya udhalilishaji wa kijinisia yanapojitokeza katika maeneo ya miji na vijiji mkoani humo.
Akizungumza na habari hizi maalum Kuelekea kilele cha siku 16 za kupinga udhalilishaji wa kijinsia kwa wanawake na watoto duniani Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Pemba Salama Mbarouk khatib Alisema usimamizi na mashirikiano yanayoendelea kuoneshwa katika utekelezaji wa mikakati hiyo iliyowekwa imesaidia kukuza uelewa wa wanajamii ndani ya mkoa huo ambao kwa sasa wamekuwa na muamko mkubwa wa kuyaripoti matukio ya udhalilishaji katika vyombo vya sheria na kuchukuliwa hatua .
"Mara tu Nilipoteuliwa kushika nafasi hii ya Mkuu wa Mkoa Disemba 1 / 2020 nilitafakari namna gani naweza kupambana na suala la udhalilishaji wa kijinsia katika Mkoa wangu ".
"Nilianzisha kamati ya mkakati ya kushughulikia Udhalilishaji wa kijinisia kwa wanawake na watoto ambayo inashirikisha jeshi la polisi, Mahkama, Mkurugenzi wa Mashtaka, wakuu wa wilaya Wete na Micheweni, Viongozi wa Dini, Masheha, Waandishi wa Habari, maafisa kutoka Mamlaka ya kupambana na Rushwa na Uhujumu Uchumi, wizara ya Afya,kituo cha Mkono kwa Mkono, lakini pia wadau mbali mbali ambao wamo katika mapambano ya udhalilishji wa kijinsia dhidi ya wanawake na watoto ambapo kwa pamoja tumekuwa tukuchukua hatua mbali mbali za kiutendaji kila mmoja kwa nafasi yake nikiwa kama mwenyekiti wa kamati hiyo lengo ni kupunguza kasi ya wimbi hili la udhalilishji ili kuona linaondoka katika Mkoa wetu".
Mkuu huyo Alitaja hatua hizo za kiutendaji ambazo zinazoendelea kuchukuliwa na kamati hiyo ni pamoja na kutoa elimu kwa wananchi kwa kufaya mikutano inayozungumzia masuala ya udhalilishaji, kufuata maelekezo ya serikali Kuu kuelekeza nguvu ya kulimaliza suala la udhalilishaji kwa pamoja, kuhamasisha jamii kuyatolea taarifa matendo ya udhalilishaji yanapojitokeza, kutolea ushahidi na kufika mahakamani baada ya kujtokeza matokeo ya udhalilishaji lakini pia kuepuka muhali na kuwaficha wahalifu wanaofanya matendo ya udhalilishaji.
"Mikakati ilisimamiwa na inaendelea kusimamiwa vyema kila mmoja kwa nafasi yake jambo ambalo limepelekea kuongezeka idadi ya matukio ya vitendo vya ubakaji na ulawiti, ambavyo vinaripotiwa ukilinganisha na miaka iliyopita nyuma wananchi walikuwa hawayaotolei taarifa kutokana na kukosa uelewa juu ya atahari ya vitendo hivyo ."
" Wanaotenda makosa hayo wanashtakiwa na sheria zinapowatia hatiani wanapewa adhabu kwa mujibu wa makosa yao wapo amba wanatumikia chuo cha mafunzo cha miaka 30 wapo miaka 15 ni kwa mujibu wa sheria ilivyowatia hatiani,hii ni moja kati ya mafanikio makubwa yaliofikiwa ya kupambana na vitendo hivi katika Mkoa wa kaskazini Pemba".
Aidha alisema kuwa Mikakati mengine iliyowekwa katika kamati hiyo ni kusimamia ufikishwaji wa kesi katika vituo vya polisi na kusimamia kufunguliwa majadala ili ziweze kufikishwa kwa mkurugenzi wa mashtaka na kuweza kufikishwa Mahakamani pamoja na kusimamia ili kuhakikisha zinafanyiwa uchunguzi.
Hata hivyo Salama Amewataka madakatari wanaofanya uchunguzi kwa watoto wanaofanyiwa udhalilishaji kutoa ushahidi juu ya kile ambacho wamekiona na kuacha tabia ya kusema kuwa ni wazoefu ili kuharibu ushahidi.
Alieleza kuwa Kamati hiyo itaendelea Kushirikiana na taasisi binafsi pamoja na serikali katika kuona kesi hizi hazikai kwa muda mrefu kupatiwa hukumu zinapofika mahakamani.
Aidha mkuu wa mkoa huyo alisema kuwa kamati hiyo inaendelea na utaratibu maalum wa kufanya tathmini ya hatua zilizofikiwa katika mapambano hayo ambapo alisema Mkuu wa mkoa huyo Alisema kuwa mpka sasa kamati mkakati hiyo imefanikiwa kwa kiasi kikubwa kupunguza vitendo vya udhalilishaji ikiwemo mimba za umri mdogo.
Aidha Aliwataka wanakamati na wananchi katika mkoa huo kusimamia wajibu wao katika mapambano hayo ili kuendelea kubaini kasoro zilizopo ambazo zinahitaji kuchukuliwa hatua katika kumaliza vitendo vya idhalilishaji.
"Kila mmoja kwa nafasi yake atimize wajibu wake tutaweza kuona kipi kinahitaji nguvu ya ziada katika kuendeleza mapambano haya ili yamalizike katika mkoa huu.
Nao baadhi ya wananchi katika Mkoa huo Wamemshukuru Mkuu wa mkoa huyo kwa jitihada anazoendelea kuzifanya katika kupambana na vitendo vya udhalilishaji ambapo wamesema jamii imeanza kuelewa madhara ya udhalilishaji, rushwa muhali jambo ambalo limebadilisha uelewa kwa wanajamii waliowengi na kuendelea kuyaripoti yanapojitokeza.
Harakati za kupata takwim sahihi juu ya mwenendo wa kesi za udhalilishaji katika mkoa huo zinaendelea .
Mwisho.
- Get link
- X
- Other Apps
Comments
Post a Comment