MJUE MWANAMKE WA KWANZA KUONGOZA KASKAZINI PEMBA HAIJAWAHI KUTOKEA NI IPI SIRI YAKE!.

AMINA AHMED –PEMBA .

  

“...Mwenyezi Mungu amewaumba kutokana na nafsi moja...” (7:189)

Wajibu na majukumu ya mwanamke ni kama ya mwanamume, na suala lake ni
kama la mume yaani suala la haki, ujumbe na marejeo. Isitoshe,
mustakbali wa kazi yoyote ni dini kwa njia moja au nyengine mwanamke
naye ana kazi yake.

Kuna kazi zingine ambazo hakuna awezaye kuzisimamia na kuzitekeleza
ila yeye, kwa maana hiyo, huwezi kupata harakati zozote zenye kufaulu
ila mwanamke atakuwa na fungu lake kubwa humo.

“...Lau si waumini wanaume na waumini wanawake...” (48:25)

Kazi inayompasa kufanya mwanamke wa kidini siyo zawadi anayopewa na
mwanamume (akikataa kumpa, basi) bali ni miongoni mwa haki zake na ni
miongoni mwa majukumu yake kwa hiyo ni juu yake atekeleze majukumu
yake.

Vinginevyo, hatakubaliwa atoe udhuru mbele ya Mwenyezi Mungu na
Historia kwamba wanaume hawakumwachia atimize wajibu wake wala
hawakumpa kazi ya kufanya kwenye utekelezaji huo.

Kwa hivyo ni lazima mwanamke huyo ajihisabu kuwa yumo kwenye
kutekeleza wajibu wake kwa kujitolea nafsi yake kwenye upande wa
mapambano kwa kuinua kiwango chake cha kifikra, kisiasa, kielimu,
kidini na kikazi.

Itoshe kuelezea umuhimu wa mwanamke katika Uislamu bali shauku yangu
ni kumuelezea  Mkuu wa mkoa wa Kaskazini Pemba Salama Mbarouk Khatib
ambae ni kiongozi mwanamke ambae sio rahisi kupata mfano wake katika
utendaji kazi, uthubutu lakini pia ujasiri alionao.

Unapozungunzia mkuu wa  mkoa  mwanamke kwa Pemba huwezi kuliacha jina
la Salama Mbarouk Khatibu kutoka na harakati zake za Uongozi na
aliedumu kwa muda mrefu katika Uongozi tokea awamu ya saba ya Serikali
ya Mapinduzi Zanzibar.

Kiongozi huyu mwanamke anachukuwa mfano wa Mwanamke Hajar na Ibrahim (A.S)

Ambae alikuwa  Mwanamke jasiri, mwenye nia safi aliyeihama nyumba yake
na nchi yake ili aende akaishi kando ya nyumba ya Mungu katika ardhi
kame isiyo na maji wala manyasi ili amwabudu Mungu pekee na ajitenge
na kuabudu watu.

Mfano huo ndivyo ulivyo kwa RC mama Salama Mbarouk Khatibu pale
anapoamuwa kutekeleza majukumu yake ya uongozi ndani ya mkoa wa
Kaskazini Pemba kwa vile hajali muda , juwa wala mvua ili akamilishe
lile alilopangiwa na Viongozi wake wakuu kwa mustakbali wa kuleta
maendeleo ya wananchi wa mkoa huo.

             
 SALAMA MBAROUK KHATIB   RC  / KASKAZINI PEMBA. 

Makala hii maalum  ilifunga safari hadi katika Ofisi za  Mkoa wa
kaskazini Pemba alipo Mkuu wa mkoa Salama Mbarouk Khatib , lengo ni
kutaka  kukujuza kiundani     mwanamke  huyo  mfano wa kuigwa  na
wanawake wengine wanaotaka  kuwa  viongozi bora  na wenye kuleta
maendeleo katika  jamii .

Baada ya kufika katika Ofisi hizo licha ya majukumu mengi  aliyokuwa
nayo  lengo liliweza kufikiwa baada ya kufanikiwa kupata  kutenga
muda  maalum kiongozi huyo  na kutoka mashirikiano  juu ya lile lengo
lililokusudiwa na makala hii.

Salama Mbarouk Khatib   ni mwanamke pekee aliteuliwa kuongoza
mkoa wa kaskazini  kwa mara ya kwa za kati ya wakuu wa mikoa 14
waliopita kabla yake.

Lakini pia  ni Mwanamke pekee  alieteuliwa kuongoza mkoa kati  ya
wakuu wa mikoa watano waliopo Zanzibar katika  awamu ya nane ya Rais
Dk, Hussein Ali.

Serikali ya awamu ya nane ilivyoweza kumuamini mwanamke na kumpa
nafasi mbali mbali za uongozi na ikiwa ni pamoja na kuongoza mikoa,
Wizara  pamoja na taasisi mbali mbali huku ikiwa  na katiba zote mbili
ya Jamhuri wa Muungano wa Tanzania na ya Zanzibar zimempa nafasi sawa
mwanamke  50 kwa 50 ya uongozi wanawake na wanaume  huku zikitekeleza
mkutano wa azimio la  mkutano wa Beijing uliofanyika nchini China
takriban miaka 26 iliyopita.

Zanzibar  ina jumla ya mikoa mitano   mitatu kati ya hiyo  inapatika
katika kisiwa na Unguja ambayo ni  Mkoa wa  mjini Magharibi, Mkoa wa
Kusini na Kaskazini Unguja  huku kwa upande wa kisiwa cha Pemba ni
Kusini na kaskazini Pemba.

"Mh, Rais  kwanza kafanya jambo kubwa na la maana kwa upande wangu
nimshukuru kwa dhati  kwa kuniandikia historia   hii maishani kwangu,
lakini pia kuniandikia historia  mpya kaskazini Pemba,” alieleza.

Alisema yeye ni mkuu wa mkoa wa 15 kwa mujibu wa uteuzi , lakini
katika wakuu wa mikoa 15 wote waliopita walikuwa ni wanaume jambo
ambalo linaonesha mabadiliko na  wanawake wenzake na hakuna cha
kuogopa ni muda wa mabadiliko sasa kikubwa ni kuona  utendaji kazi
unafanyika .

Harakati za  Salama Mbarouk Khatib zilianza mbali  ambapo alisema
kuwa" siri kubwa  niwaambie wanawake wenzangu kikubwa ni kujiamini na
tunapopata nafasi inatubidi tuitendee haki ipasavyo”, alieleza.
 
" Harakati zangu mimi zilianza mbali sana lakini siri kubwa ilikuwa ni
uthubutu  nimekuwa natumia fursa ipasavyo ninapoipata  niliwahi kuwa
mkuu wa wilaya Chake Chake nikawa mkuu wa wilaya  ya Micheweni na mote
humo nilisimama kama kiongozi wala sikusimama  kuhofia jinsia katika
utendaji wangu wa majukumu ", alisema RC.

Mashaallah, Allah amjaalie mafanikio mema,  wepesi na utayari  wake
katika utendaji kazi kabla ya kuteuliwa kuongoza nafasi hiyo
kumechangia kufika hapa alipo sasa ambapo kwani aliweza kuhudumu
katika nafasi mbali mbali wakati akiwa katika Wizara ya Wanawake na
watoto kwa sasa Ustawi wa jamii kama Ofisa Mipango.

" Nilikuwa najiamini na naitendea haki kazi niliopewa sekta
niliyopangiwa sikuwa na hofu wala woga  pakutolewa maamuzi kama
kiongozi nilikuwa natoa, pakushauri nilikuwa nashauri  pia nilikuwa
nasikiliza na kufanyia kazi maelekezo,  na kufuata Sheria , Sera
pamoja na , miongozo ya serikali  lakini  zaidi sikuwa na hofu  nahisi
hicho ndio kitu kilichopelekea leo kufika hapa nilipo", alisema.

Alieleza kuwa jukumu la uongozi alilonalo huku akiwa ni mke lakini pia
mama wa familia  linatofautishika   haliyaathiri utendaji kazi, hivyo
ni kusema maisha ya uongozi hayaathiri  familia yake bali yanaongeza
heshima na  mashirikiano jambo ambalo linazidi kumpa ari na nguvu ya
kufanya kazi kwa bidii.

" Mimi ni mama ambae nina mume na nina watoto serikali inanitegemea
lakini niseme kwamba kikubwa ni kujifahamu tu , unapokuwa Serikalini
wewe ni kiongozi ujuwe wewe ni kiongozi na unapokuwa nyumbani ujuwe
wewe ni mama ambae unastahiki kufanya majukumu yako na mimi nafanya
hivyo bila usumbufu wowote “, alieleza RC .

Alindelea kusema  kuwa kama mama ana watoto wadogo huku ni mkuu wa
mkoa  ambapo watoto wanataka huduma ya mama zaidi na mara nyingi
inakuwa anasafiri, kazi ni nyingi zaidi, lakini na wao wanajuwa kama
ni mama  yao kwani anakuwa anajipanga a natoa  mashirikiano  nakuwa
karibu nao  kila anapokuwa nyumbani.

Hata hivyo Bi Salama  aliwataka wanawake wengine nchini kusimamia
maamuzi yao bila kuogopa vitisho ili kuonesha uwezo walionao katika
utendaji kazi.



" Katika kuwaaminisha wananchi  kuamini utendaji kazi wako ni
kusimamia malengo yako na kutokukubali kurudishwa nyuma jambo hilo
litawafanya waweze kujenga imani ya kukuamini wewe unaweza kuongoza
bila kujali jinsia”, alieleza.

 Anaeleza kuwa wananchi wameamka sasa hivi hawaangalii jinsia
wanaangalia utendaji kazi  aliwaasa wanawake wenzake kutuogopa fursa
wasizichezee watufanye kazi kadri ya uwezo wao na suala hilo linaweza
kuwapa fursa wanawake kupata nafasi zaidi ya ukuu wa mkoa na
nyenginezo.

 Alifahamisha licha ya watu wachache kumtia midomoni katika utowaji wa
maamuzi ya kiutendaji   katika uongozi wake bi Salama hakulipokea
suala hilo kama ni kikwazo kwa upande wake anajiamini.

" Kuna baadhi ya watu wanaotaka wakuendeshe vile wanavyotaka wao kwa
maslahi yao binafsi jambo ambalo kwangu silipi kipaumbele naamua kwa
kufuata sheria   na miongozo  kwa maslahi ya taifa wao wanaishia
kunitupia majungu bi salama mkali haambiliki”, alifahamisha.

" Unapofanya kazi ndipo kasoro zinaonekana na ukikosa kasoro wewe sio
binaadamu kwahiyo nakubali kushauriwa  lakini zaidi na  angalia ule
ushauri ninaopewa je hautokweda kinyume na sheria za serikali,  jee
una maslahi ya taifa, hautoathiri serikali ndipo naufanyia kazi
kikubwa ninachoangalia ni hicho", alisema.

Alieleza kuwa elimu inanafasi  na na mchango mkubwa katika kuwa
kiongozi bora mbapo aliwataka wanawake kuendelea kusoma na kujifunza
mambo mbali mbali.

Alisema licha ya mashirika kupigania Women mwananmke na Uongozi  bado
wanawake  wengine hawajajua lengo la kupigania kupata haki hizi kuwa
ni kupata haki  zetu ipasavyo ili wanawake kupata maendeleo.

Mgeni Khatib Yahya mkuu wa wilaya ya Micheweni alisema kuwa  kiongozi
huyo ndie ambae alikuwa anajifunza mambo mengi kutoka kwakwe kabla ya
hajawa mkuu wa wilaya na hadi sasa anaendelea kupata ushauri na
kupokea mawazo  mbali mbali kutoka kwa  kiongozi wake huyo.

"Najifunza siku hadi siku mambo mazuri  kutoka kwa Mh Salama
ananishauri ananipa maelekezo  kama msaidizi wake na natekeleza
majukumu yangu vyema kwa kufuata nyao zake zaidi nakubali uthubutu  na
namna anavyojiamini katika uongozi wake ,tunasaidiana kwa pamoja
kuleta maendeleo  kumsaidia Rais wa Zanzibar , "anaeleza.

Wakizungumza baadhi ya wakaazi wa wete   waliozungumza na makala hii
juu ya uongozi wa mkuu huyo wa mkoa akiwemo  Bi Aziza Makame Abass
Mkaazi wa  Limbani  wilaya ya hiyo alisema kuwa  jitihada zinazofanywa
na mku huyo wa wilaya katika kuleta maendeleo ya mkoa huo yanaonekana
na kila mtu ambapo aliiomba Serikali kumuacha aendelee kuishikilia
nafasi hiyo kwa miaka yote.

"Kwanza binafsi nampenda anavyofanya kazi  nikisikiliza radio jamii
nisipomsikia jioni basi asubuhi nitamsikia    anazungumzia  jambo
lolote  tunajuwa hasa wa kama tuna kiongozi   sio wengine ambapo hata
kuwasikia kwa radio hatuwasikii  anajitahidi  Rais asituondolee tunu
hii  wazazi   tunaojuwa tunaifurahia”,  alisema.

" Kile ni kipaji   wanawake wengine wajifunze pale mana ni darasa  la
namna ya mwanamke atakapoamua kuwa kiongozi  vipi anatakiwa awe
kabisa,” alisema .

Mwananchi Salim Ali wa Wete ,anasema anazipongeza juhudi za kupata
viogozi wanawake zilizochukuliwa na mashirika na asasi mbali mbali
zilizopigania  na zinazoendelea kumpigania mwanamke kupata haki na
fursa sawa katika  uongozi ambapo  ni pamoja Chama Cha waandishi wa
Habari  wanawake Tanzania TAMWA  Tanzania na Zanzibar.

Anafahamisha kuwa Zanzibar kwa sasa  kasi ya wanawake kuingia katika
uongozi imeongezeka ukilinganisha  na miaka iliyopita ambapo kwa
mujibu wa takwimu  fupi iliyotolewa na Chama cha waandishi wa Habari
Tanzania TAMWA Zanzibar  zilionesha kuwa  idadi ya viongozi wanawake
katika Baraza la wawakilishi ni asilimia  36 ambayo ni sawa na
wanawake 28  kati ya wawakilishi 84 waliopata  nafasi hiyo.

Anaeleza kwa Takwimu hizo bado  haitoshi na wanawake hawajapata fursa
sawa za usawa wa kijinsia katika vyombo vya kutolea maamuzi  utawala
na utowaji wa maamuzi katika ngazi za maamuzi.

BiSalama ametowa wito kwa wanawake wote nchini ambapo amewataka
kutotumia vibaya madaraka wanayoyapigania kuyapata   badala yake
wayatendee haki, kwa kufanya kazi vizuri, kuwashirikisha wengine,
ujitathmini na kujiuliza masuali katika kila hatua ya utendaji.

"Tuige mazuri kutoka kwa wanawake wengine binafsi mimi ni mwanamke
pekee yangu lakini wakuu wa mikoa wenzangu ambao ni wanaume  wanasema
katika vikao.

" Yule ni mwanamke lakini  anapambana  na mimi nilikuwa sijui hizi
taarifa lakini wanakuwa wanaiambia wengine wananipa hongera wengine
wananipigia kutaka ushauri wa kuleta maendeleo katika mikoa yao kwa
hiyo kimeeleweka kwamba kumbe mkuu wa mkoa wa kaskazini ni mwanamke
lakini anapambana na juhudi zinaonekana kwamba wanawake tunapopewa
fursa tunaweza kufanya kazi”, anaeleza .

Ni  Wanawake 22 pekee ambao ni viongozi wakuu  kati ya nchi   na
mataifa ya  nchi 123 kwa idadi hiyo bado jitihada zinahitajika katika
kuona mwanamke anapata fursa sawa katika vyombo vya maamuzi ili kupata
idadi kubwa zaidi Zanzibar naTanzaniabara  pamoja na Mataifa mbali
mbali.

Hata hivyo kuna usemi kuwa “Hakuna kinachoshindikana chini ya jua”
usawa wa kijinsia katika ngazi ya maamuzi Uchumi, Siasa, Biashara,
elimu  na majukumu ya kiutendaji inawezekana iwapo wanawake watapata
fursa sawa 50 kwa 50.



                                    MWISHO.

Comments

Popular posts from this blog

BARABARA 19 KUJENGWA KWA KIWANGO CHA LAMI PEMBA KUKAMILIKA DISEMBA 2024.

WAZAZI ZIDISHENI KUFUATILIA NYENENDO ZA WATOTO HUSUSAN NI VIJANA .

UONGOZI WA WILAYA CHAKE CHAKE KFHI WAPONGEZA JUHUDI